Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kutoka wizara zote za serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamekutana hii leo (02 Januari, 2016) katika ukumbi wa Mikutano wa Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata semina elekezi iliyoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mada zilizoandaliwa katika semina hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, amesema semina hiyo ni ya kikazi zaudu na kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu hao ambao waliapishwa jana wanatekeleza wajibu wa kusimamia utendaji kazi wa serikali vizuri.
Balozi Sefue ameelekeza kuwa kila Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu anapaswa kutambua kuwa nafasi yake ni ya maamuzi, hivyo serikali inatarajia kuona kuwa daima anafanya maamuzi kwa usahihi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazomuongoza katika majukumu yake.
Aidha, ameonya kuwa serikali ya awamu ya tano inawatarajia viongozi hao kuwa watakuwa wasimamizi wazuri wa fedha za umma na kwamba haitarajii kuwepo kwa hati za ukaguzi wa mahesabu zenye kasoro.
Balozi Sefue ameongeza kuwa Makatibu Wakuu hao na Naibu Makatibu Wakuu ni mamlaka ya nidhamu katika wizara zao, hivyo Serikali haitarajii kuona wanakua na kigugumizi katika kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaokuwa na makosa, na akakumbusha kuwa haikubaliki kwa mtumishi aliyefanya makosa katika sehemu moja ya kazi, kuhamishiwa katika sehemu nyingine badala ya kuchukuliwa hatua palepale alipo.
Semina hii elekezi imefanyika kwa siku moja