Ligi Kuu soka Tanzania bara imeendelea tena leo February 3 kwa michezo mitano kupigwa katika viwanja tofauti tofauti Tanzania, klabu ya Dar Es Salaam Young Africans ilikuwa mgeni wa klabu ya Tanzania Prisons uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati watani zao wa jadi Simba walikuwa wenyeji wa Mgambo JKT uwanja wa Taifa Dar Es Salaam
Simba ambao kwa sasa wapo na kocha wao msaidizi Jackson Mayanja bila kuwa na kocha mkuu wamefanikiwa kuendeleza hali ya ushindi kwa kila mechi, baada ya mchezo wao wa wiki iliyopita dhidi ya Africans Sports kuibuka na ushindi wa goli 4-0. February 3 Simba wamefanikiwa kuibuka na ushindi mwingine mnono dhidi ya Mgambo JKT uwanja wa Taifa, kwa kuwafunga idadi ya goli 5-1.
Wekundu wa Msimbazi Simba walikuwa mahiri katika kuuchezea mpira, kwani dakika ya 5 tu walifanikiwa kupachika goli la kwanza kupitia kwa Hamis Kiiza, kabla ya Mwinyi Kazimoto hajafunga goli la pili dakika ya 28 na Ibrahim Ajib kufunga goli la tatu dakika ya 45. Kipindi cha pili Simba waliendeleza ubabe baada ya dakika ya 77 Danny Lyanga kupachika goli la nne
Mshambuliaji wao tegemeo Hamis Kiiza alihitimisha ushindi huo kwa kufunga goli la tano, Mgambo walipata goli la kufutia machozi dakika ya 87 kupitia kwa Fully Maganga baada ya ngome ya ulinzi ya Simba kujisahau. Kwa matokeo hayo Simba wanakuwa nafasi ya pili wakiwa na point 39 nyuma ya Yanga kwa tofauti ya point moja
Matokeo ya mechi nyingine za Ligi Kuu zilizochezwa February 3
• Prisons 2 – 2 Yanga
• Kagera Sugar 2 – 1 Majimaji FC
• Africans Sports 1 – 0 Mwadui FC
• Mtibwa Sugar 2 – 2 Toto Africans