Ugonjwa wa kansa una ishara nyingi ambazo hutegemea zaidi kansa hiyo ipo kwenye sehemu gani ya mwili, imekwisha enea kwakiwango gani na ukubwa wa uvimbe wa kansa hiyo. Kansa nyingine huonekana kwa macho au kwa kupapasa juu ya ngozi – uvimbe juu ya ziwa au kwenye korodani huweza kuwa ishara ya kansa. Kansa aina ya melanoma mara nyingi hutambuliwa kutokana na mabadiliko ya vijipele juu ya ngozi. Kansa nyingine hutoa mabaka meupe ndani ya midomo au madoa meupe kwenye ulimi.
Kansa nyingine hutoa dalili ambazo hazionekani dhahiri. Uvimbe wa kwenye ubongo, mathalani, huathiri jinsi mtu anavyoweza kutambua vitu na kansa za kwenye kongosho hazitoi ishara mapema hadi maumivu yatakapoanza pale neva za maeneo ya karibu zitakapoanza kuminywa au shughuli za ini zitakapoathiriwa na
kusababisha ngozi na macho kuwa ya rangi ya njano (jaundice). Ishara nyingine zitaonekana uvimbe utakapoanza kusukuma viungo vya karibu au mishipa ya damu. Kwa mfano, kansa za kwenye utumbo huweza kusababisha kukosa choo kikawaida, kuharisha au kiasi cha kinyesi kinachotolewa. Kansa za tezi dume huathiri ufanyakazi wa kibofu cha mkojo na kusababisha kupta haja ndogo mara kwa mara au kutopata haja ndogo.
Kwa vile seli za kansa hunyonya nguvu za mwili na kuvuruga mfumo wa kinga za mwili, ishara nyingine za homa, uchovu, kutokwa jasho, kukosa damu, kupungua uzito kusiko na sababu huweza kutokea.
Kansa iliyoenea hadi kwenye maeneo ya ubongo husababisha kizunguzungu na maumivu ya kichwa. Kansa ya mapafu inawezaa kusababisha kukohoa na kupumua kwa shida. Ini linaweza kuwa kubwa na kusababisha ugonjwa wa homa ya manjano, mifupa huweza kuuma na kuvunjika kirahisi.